Kuwekeza Katika Maisha ya Watu wa Kenya: Kuthamini Manufaa ya
Uhusiano Kati ya Marekani na KenyaSura ya Pili (Sehemu ya 1 ya 3)
Sura ya PiliJe, ni jinsi gani serikali ya Marekani inachangia katika ustawi
wa Kenya?
Kenya ni mshirika wa kimkakati na rafiki wa Marekani katika kukuza
amani na usalama kote katika kanda ya Afrika Mashariki. Mnamo
2020, nchi hizo mbili zilisherehekea miaka 57 ya mahusiano ya
kidiplomasia ambayo yanawezesha ushirikiano wa kiuchumi na wa
kimaendeleo, pamoja na ushirikiano katika masuala ya usalama.
Serikali ya Marekani inasaidia katika ukuaji na ustawi wa Kenya
kwa njia tatu muhimu: (1) msaada kati ya nchi mbili, (2) msaada wa
kimataifa, na (3) ukuzaji wa mazingira mazuri ya kubuni sera za
kuwezesha biashara, uhamiaji, na uwekezaji.
Kwa jumla, tunakadiria kwamba msaada unaoendeshwa na serikali ya
Marekani huchangia takriban Dola bilioni 1.68 kila mwaka katika
uchumi wa Kenya. Hiyo inajumuisha Dola bilioni 1 katika msaada wa
moja kwa moja kati ya nchi mbili na msaada wa kimataifa kwa mwaka
kwa wastani, na pia Dola milioni 678 katika michango isiyo ya moja
kwa moja kutoka kwa sera saidizi. Katika sehemu iliyosalia ya sura
hii, tunachunguza kila moja ya njia hizi tatu ili kuelewa jinsi
zinavyofaidi raia wa Kenya.
Sehemu ya 2.1Michango ya moja kwa moja ya serikali ya Marekani kuelekea
Kenya
Msaada rasmi wa maendeleo (Official Development Assistance, ODA) —
pamoja na misaada ya kifedha, mikopo yenye masharti mazuri, na
ushauri wa kiufundi — ni njia muhimu zinazotumiwa na serikali ya
Marekani kusaidia katika ukuaji na ustawi wa Kenya. Marekani
kihistoria imekuwa mshirika mkubwa zaidi wa Kenya katika maendeleo
kwa msingi wa kuzingatia mtiririko wa jumla wa msaada kutoka kwa
shirika la ODA (OECD-DAC, n.d.). Isitoshe, serikali ya Marekani
imekuwa ikiongoza katika kutoa msaada kwa mashirika ya kimataifa
(k.m. mashirika ya Umoja wa Mataifa, benki za maendeleo) na kwa
hazina za wafadhili wengi zinazofanya kazi nchini Kenya. Katika
sehemu hii, tunachunguza jinsi msaada kati ya nchi mbili na msaada
wa kimataifa wa Marekani inavyoshirikiana kusaidia raia wa Kenya
kuafikia malengo yao yaliyoanishwa katika Ruwaza ya 2030.
Kilichogunduliwa 1:Serikali ya Marekani ilichangia takriban Dola milioni 931 kwa
wastani katika msaada kati ya nchi mbili kila mwaka kwa Kenya
kwa miaka mitano iliyopita, hasa katika sekta ya afya.
Mawakala na idara ishirini za serikali ya Marekani zimechangia
moja kwa moja katika ukuaji na maendeleo ya Kenya tangu 2001.[4]
Kati ya hayo, Wakala wa Marekani wa Maendeleo ya Kimataifa (USAID)
unaongoza juhudi za Marekani za kati ya nchi mbili katika nyanja
muhimu kama vile: kilimo na uhakika wa chakula, elimu, afya,
kufanikisha serikali ya ugatuzi kwa faida ya wote, ukuzaji wa
amani, mazingira, na ukuaji endelevu wa uchumi (USAID Kenya, n.d).
Kati ya 2001 na 2018, serikali ya Marekani iliongeza msaada wake
wa kila mwaka kati ya nchi mbili kwa Kenya mara kumi, kutoka Dola
milioni 106 hadi Dola milioni 986.54 (tazama
Mchoro wa 1).[5]
Katika miaka mitano iliyopita,[6]
Marekani imechangia kwa wastani Dola milioni 931 kwa mwaka katika
msaada kati ya nchi mbili.
Mchoro wa 1.Msaada kati ya nchi mbili kutoka kwa serikali ya Marekani
kwenda Kenya, 2001-2018
↩
Notes: This graph visualizes total U.S. government bilateral
assistance disbursements to Kenya each year from 2001 to 2018 in
constant USD 2019. These figures include both development
assistance and security aid directly given via U.S. government
agencies. They exclude assistance given by the U.S. via
multilateral agencies that may also benefit Kenya.
Source: USAID Foreign Aid Explorer Data (2001-2018).
Asilimia sitini na mbili ya msaada kati ya nchi mbili kutoka
Marekani kwenda Kenya kati ya mwaka wa 2010 na 2018 ililenga sekta
ya afya (tazama
Mchoro wa 2). Msaada huo unasaidia katika kuimarisha juhudi za serikali ya
Kenya katika kutoa huduma za afya za bei nafuu kwa wote. Kwa
mfano, mnamo 2017, jumla ya msaada kati ya nchi mbili kutoka
serikali ya Marekani ulioenda katika sekta ya afya ulikuwa Dola
milioni 598.7. Msaada huo uliongezwa katika kiasi cha Dola milioni
367.5 ambazo Kenya ilihamasisha kutoka vyanzo vya ndani ya nchi
ili kukidhi mahitaji yake katika sekta ya afya (Hazina ya Kitaifa,
2017).
Mchoro wa 2.Msaada kati ya nchi mbili uliotolewa kwa Kenya na serikali ya
Marekani katika sekta mbalimbali, 2010-2018
↩
Maelezo: Grafu hii inaonyesha kwa mtazamo wa sekta jumla ya
msaada kati ya nchi mbili uliotolewa na serikali ya Marekani kwa
Kenya kutoka 2010 hadi 2018 kwa msingi wa thamani isiyobadilika
ya Dola ya 2019.
Asili: USAID Foreign Aid Explorer Data (2010-2018).
Serikali ya Marekani hutoa sehemu kubwa ya msaada wake katika
sekta ya afya kuisaidia Kenya kupambana na janga la HIV/UKIMWI.
Serikali ya Marekani ndio mfadhili mkubwa zaidi wa mipango ya
kuzuia HIV na UKIMWI nchini Kenya (tazama
Kikasha cha 1). Isitoshe, Marekani pia imeongeza ufadhili wake tangu 2008
(tazama
Mchoro wa 3) kusaidia Kenya kushughulikia masuala mengine ya afya ya
kipaumbele, kama vile: kifua kikuu, ugonjwa wa malaria, upangaji
uzazi na afya ya uzazi, afya ya mama na watoto, na vitisho
vinavyoibuka vya magonjwa ya kuambukiza.
Mchoro wa 3.Msaada kati ya nchi mbili uliotolewa kwa Kenya na serikali ya
Marekani katika sekta ya afya, 2001-2018
↩
Maelezo: Grafu hii inaonyesha jumla ya msaada kati ya nchi mbili
uliotolewa na serikali ya Marekani kwa Kenya kila mwaka kutoka
2001 hadi 2018 kwa msingi wa thamani isiyobadilika ya Dola ya
2019. Takwimu hizi zinajumuisha misaada ya maendeleo na misaada
ya usalama iliyotolewa moja kwa moja kupitia mawakala wa
serikali ya Marekani. Hazijumuishi msaada ambao huenda ulifaidi
Kenya uliotolewana Marekani kupitia mawakala wa kimataifa.
Asili: USAID Foreign Aid Explorer Data (2001-2018).
Mbali na kuunga mkono vipaumbele vya maendeleo vya muda mrefu vya
Kenya kulingana na Ruwaza ya 2030, serikali ya Marekani
ilihamasisha msaada wa dharura kusaidia watu wa Kenya kupona
kutokana na mshtuko, kama vile kuelekeza Dola milioni 95.6 katika
msaada wa chakula kwa Wakenya zaidi ya milioni 4.4 walioathiriwa
na Ukame wa Afrika Mashariki wa 2011- 2012 (tazama
Kikasha cha 2). Katika
Kikasha cha 3, pia tunachunguza kwa makini Dola takriban milioni 85.8 za
msaada kati ya nchi mbili kutoka Marekani ambao ulilenga kuwekeza
katika idadi inayoongezeka ya vijana wa Kenya kati ya 2009 na
2018.
Kikasha cha 1.Kupambana na HIV/UKIMWI nchini Kenya kupitia utafiti na
mipango ya jumla
↩
Ufadhili wa HIV/UKIMWI umekuwa sehemu muhimu ya msaada kati ya
nchi mbili kwenda Kenya kufuatia uzinduzi wa Mpango wa Dharura
wa Rais wa Msaada wa Ukimwi (PEPFAR) mnamo mwaka wa 2003. Hata
hivyo, leo, mwitikio wa Marekani umebadilika ili kujumuisha
mipango kadhaa, kama vile mpango wa Msaada Jumuishi wa UKIMWI,
Idadi ya Watu, na Afya (APHIAplus) ambayo inachukua mtazamo wa
jumla katika masuala ya afya kwa kuchanganya upangaji uzazi,
afya ya mama/mtoto, lishe na kuzuia malaria na kifua kikuu ili
kujenga mpango mpana zaidi wa huduma za afya kwa kushirikiana na
maafisa wa afya wa Kenya. Ikitoa msaada wa kifedha wa zaidi ya
Dola milioni 400 kila mwaka, Marekani imesalia kuwa mfadhili
mkubwa zaidi wa mpango wa HIV/ UKIMWI nchini Kenya, imezidi
wafadhili wengine wote wakiwekwa pamoja.
Ufadhili wa HIV/UKIMWI nchini Kenya kwa mtazamo wa wafadhili,
2009-201
Maelezo: Chati hii inaonyesha wafadhili wakubwa zaidi wa Kenya
wa kutoa msaada kati ya nchi mbili na msaada wa kimataifa
katika kuzuia HIV/UKIMWI na kugharamia matibabu kati ya
2009-2018 kwa msingi wa thamani isiyobadilika ya Dola ya mwaka
wa 2019.
Asili: OECD CRS Database (2009-2018).
Mbali na kufadhili mipango ya afya ya umma nchini Kenya, Idara
ya Ulinzi ya serikali ya Marekani pia inasaidia katika
utekelezaji wa utafiti muhimu juu ya magonjwa ya kuambukiza
nchini Kenya. Taasisi ya Utafiti wa Kimatibabu ya Kenya (KEMRI)
imekuwa mwenyeji wa Kitengo cha Utafiti wa Kimatibabu cha Jeshi
la Marekani (USAMRD) tangu 1969. Kwa karibu miongo mitano ya
kuendesha shughuli zake, maabara hiyo ya utafiti iliyoko jijini
Nairobi, na pia vituo vyake vya nyanjani vya Kisumu, Kisian,
Kombewa na Kericho, imekuwa mstari wa mbele katika utafiti wa
kibaiolojia na kimatibabu ambao umechangia katika utengenezaji
wa chanjo muhimu na dawa za kutibu magonjwa kama vile malaria,
malale, leishmaniasis, HIV/UKIMWI, na virusi vinavyosambazwa na
wadudu kama mbu na kupe.
Kikasha cha 2.Kutoka hali za dharura za njaa hadi kufikia uhakika wa
chakula. ↩
Kati ya mwaka wa 2008 na 2018, serikali ya Marekani ilitoa
takriban wastani wa Dola bilioni 1.2 (wastani wa Dola milioni
109 kwa mwaka) katika kusaidia kupambana na njaa nchini Kenya
chini ya Kifungu cha II cha Sheria ya Marekani ya Chakula kwa
ajili ya Amani. Hapo awali, msaada huu ulitilia mkazo utoaji wa
moja kwa moja wa chakula kinachozalishwa na Marekani kwa wale
walio kwenye hatari ya njaa au kufa njaa. Ingawa misaada mingi
ya chakula kutoka Marekani ilitolewa wakati wa Ukame wa Afrika
Mashariki wa 2011-2012, Marekani bado ilitoa wastani wa Dola
milioni 70.5 kwa mwaka kwa Kenya katika msaada wa chakula chini
ya Kifungu cha II kati ya mwaka wa 2014 na 2018. Kadiri ukali wa
hali ya dharura ya njaa iliyosababishwa na ukame wa 2011-2012
ilivyopungua, msaada wa Marekani umebadili mwelekeo kutoka kutoa
msaada wa chakula cha dharura hadi kuzingatia uhakika wa chakula
wa muda mrefu. Mwelekeo huu wa kuzingatia uhakika wa chakula wa
muda mrefu unalenga kusaidia jamii kupunguza hatari ya dharura
za baadaye kupitia juhudi za kuzuia utapiamlo na kusaidia
uzalishaji wa kilimo.
Utoaji wa kila mwaka wa msaada wa chakula wa Marekani chini ya
kifungu cha II na msaada wa kilimo kutoka Marekani kwenda
Kenya, 2008-2018
Maelezo: Grafu hii inaonyesha thamani ya jumla ya kila mwaka
ya msaada wa chakula chini ya Kifungu cha II kutoka Marekani
kwenda Kenya na thamani ya jumla ya kila mwaka ya msaada wa
kilimo kutoka Marekani kwenda Kenya kati ya 2008 na 2018, kwa
msingi wa thamani isiyobadilika ya Dola ya mwaka wa 2019.
Asili: USAID - Food for Peace Funding Overview Fact Sheet
(2008-2018) and USAID Foreign Aid Explorer Data (2001-2018).
Kikasha cha 3.Elimu kwa vijana, uongozi, na kujikimu kimaisha ↩
Ikiwa na asilimia 75 ya idadi ya watu walio chini ya umri wa
miaka 35 (Baraza, 2020), kuwekeza katika idadi inayozidi
kuongezeka ya vijana wa Kenya ni muhimu katika kutimiza azma ya
Kenya ya kufikia hadhi ya kuwa taifa la kipato cha kati ifikapo
2030. Kwa ajili ya hiyo, serikali ya Marekani ilihamasisha
wastani wa Dola milioni 85.8 katika msaada wa moja kwa moja kati
ya nchi mbili kutumika katika mipango inayofaidi vijana wa Kenya
kati ya mwaka wa 2009 na 2018. Uwezeshaji wa kiuchumi unaolenga
vijana ndio sehemu kubwa zaidi ya msaada huu (asilimia 37),
ikifuatiwa na mipango inayotoa makao na mafunzo ya kujikidhi
kimaisha, miongoni mwa aina nyingine za msaada, msaada kwa
wakimbizi vijana (asilimia 18), na msaada wa kupokea elimu ya
msingi na ya juu (asilimia 14).
Msaada wa serikali ya Marekani katika mipango mingi inayolenga
vijana unatilia mkazo umuhimu wa ushirikiano kati ya sekta ya
umma na ya kibinafsi kuwekeza katika kizazi kijacho cha viongozi
na wafanyakazi. Mpango wa Ajira na Ujuzi kwa Vijana wa Kenya
(The Kenya Youth Employment and Skills, K-YES) inatoa fursa kwa
viongozi wa sekta ya umma na ya kibinafsi kufanya kazi kwa
pamoja kutatua changamoto za ukosefu wa ajira kwa vijana kupitia
mipango mahususi ya mafunzo ya kazi ambayo inasaidia vijana
kujaza mapungufu ya ujuzi katika tasnia zinazolengwa. Mpango wa
The Young African Leaders Intiative (YALI), inashirikiana na
vyuo vikuu 40 vya Marekani kufunza ujuzi na kutoa msaada kwa
vijana wa Kenya kupitia mradi wake wa Mandela Washington
Fellowship Program na The Regional Leadership Centre for East
Africa (Kituo cha Uongozi cha Kanda ya Afrika Mashariki)
kilichopo Nairobi.
Maelezo: Jumla ya msaada wa moja kwa moja kati ya nchi mbili
kutoka Marekani kwenda katika miradi inayoelekezwa kwa vijana
ilikadiriwa kwa kutumia kichujio kubaini shughuli ambazo
zinataja vijana wazi kwenye jina la mradi. Hili linaweza kuwa
kadirio la chini lisilo sahihi la thamani ya jumla ya Dola za
Marekani zilizofaidi vijana wa Kenya. Takwimu zote za fedha
zilizotolewa zimewekwa kwa msingi wa thamani isiyobadilika ya
Dola ya 2019. Asili: Foreign Aid Explorer (2009-2018).