Kuwekeza Katika Maisha ya Watu wa Kenya: Kuthamini Manufaa ya
Uhusiano Kati ya Marekani na KenyaSura ya Pili (Sehemu ya 3 ya 3)
Sehemu ya 2.2Michango isiyo ya moja kwa moja ya serikali ya Marekani
kuelekea Kenya
Biashara, uwekezaji, na wafanyakazi wenye ujuzi ni viungo muhimu
katika juhudi za Kenya za kuwa taifa linalopiga hatua kwa kasi
kufikia lengo la kuwa na uchumi wa viwanda na kipato cha kati
ifikapo 2030.
[17]
Katika kila moja ya nyanja hizo, serikali ya Marekani ni mshirika
muhimu katika kuunda mazingira ya kuwezesha Kenya kuwa na uchumi
wa kisasa. Katika sehemu hii, tunachunguza jinsi sera bora za
Marekani za biashara, uhamiaji, na uwekezaji zinavyosaidia Kenya
kubadilisha uchumi wake kulingana na Ruwaza ya 2030.
Kilichogunduliwa 4:Sheria ya Maendeleo na Fursa kwa Afrika (The African Growth and
Opportunity Act) iliiwezesha Kenya kuongeza idadi ya bidhaa nje
zilizouzwa nchini Marekani kwa asilimia 285 kati ya 2000 na
2018.
Tangu miaka ya 1980, Kenya imechukua hatua nyingi ili kukuza
uchumi ulio huru kwa kubadilisha sera mbalimbali za kibiashara na
kiuchumi (Zepeda et. al., 2009). Hivi majuzi, Rais Uhuru Kenyatta
alisema kwamba Kenya inahitaji kuimarisha uzalishaji au
utengenezaji wa bidhaa viwandani na biashara nje kama mojawapo ya
vitu vinne muhimu kwenye mpango wa Ruwaza ya 2030 ya Kenya. Nchi
ya Marekani ni mshirika muhimu wa kibiashara kwa vile asilimia 8.7
ya bidhaa nje za Kenya ziliuzwa huko katika mwaka wa 2017 pekee,
nyingi kati ya bidhaa nje hizi zikitokea kwenye viwanda vya
kutengenezea nguo (WITS, n.d.).
Katika kipindi cha miongo miwili iliyopita, mapato ya Kenya
kutokana na biashara nje nchini Marekani yaliongezeka kwa asilimia
285 (tazama
Mchoro wa 6). Kuanzia 2014 hadi 2018, mapato ya Kenya ya kila mwaka kutokana
na biashara nje nchini Marekani yalikuwa takriban Dola milioni 576
kwa kukadiria. Hasa, viwanda vya nguo vya Kenya ndivyo
vilivyochangia pakubwa katika maendeleo haya, kwa vile vilichangia
zaidi ya asilimia 60 ya bidhaa nje zote zilizouzwa nchini Marekani
katika miaka ya hivi majuzi (tazama
Kikasha cha 5). Kutokana na Serikali ya Marekani kupitisha sheria nzuri za
biashara, kama vile Sheria ya mwaka wa 2000 ya Maendeleo na Fursa
kwa Afrika (the 2000 African Growth and Opportunity Act) (AGOA),
Marekani iliweza kuwa soko kubwa zaidi la ng’ambo la nguo ambazo
zimetengenezwa nchini Kenya.
Kutokana na sheria hii ya AGOA, nchi za Afrika zinazostahili au
kustahiki zinapendelewa, ikiwemo Kenya, jambo ambalo linawezesha
karibu bidhaa zote zinazoweza kuuzwa sokoni kuingia kwenye soko la
Marekani bila kutozwa kodi, zikiwemo nguo zilizotengenezwa
viwandani, ambazo ndizo zimekuwa zikiuzwa sana baada ya sheria ya
AGOA kuanza kutumika.
Sheria hii pia inaisadia serikali ya Kenya kufanikisha hatua za
maendeleo katika nyanja zinazoleta maendeleo jumuishi na uongozi
mzuri katika Ruwaza ya 2030—kukuza uchumi unaonawiri kutokana na
masoko, kuimarisha utekelezaji wa sheria, kupambana na ufisadi, na
kulinda haki za wafanyakazi—ambazo pia zinahitajika ili nchi
iendelee kustahiki au kustahili kufaidika na AGOA (Mwakilishi wa
Biashara wa Marekani).
Mchoro wa 6.Thamani ya mauzo ya nje ya Kenya kuelekea Marekani na mgawo
wa nguo, 2000-2018
↩
Maelezo: Grafu hii inaonyesha jumla ya bidhaa zilizosafirishwa
nje ya nchi na Kenya kwenda Marekani (nguzo za samawati) kati ya
2000 na 2018, na nguo kama asilimia ya jumla ya thamani ya
bidhaa zilizosafirishwa nje ya nchi na Kenya kwenda Marekani
(mstari wa samawati). Takwimu zote zimewekwa kwa msingi wa
thamani isiyobadilika ya Dola ya 2019.
Asili: World Integrated Trade Solution (WITS), The World Bank.
Kikasha cha 5. Sheria ya Maendeleo na Fursa kwa Afrika (The African Growth
and Opportunity Act) (AGOA) na kiwanda cha nguo cha
Kenya
↩
Sheria ya Maendeleo na Fursa kwa Afrika (The African Growth and
Opportunity Act) ilipitishwa ili iwe sheria na Bunge la Marekani
tarehe May 18, 2000. Sheria hii inaziwezesha nchi za kusini mwa
Sahara za Afrika zinazostahiki zinazotimiza masharti mahususi
ambayo yapo kwenye sheria hii kufikia soko la Marekani. Masharti
haya yanahitaji nchi hizi husika zijitahidi kuimarisha
utekelezaji wa sheria, haki za kibinadamu, na viwango au hali za
kazi. Hapo awali, sheria hii ilipitishwa ili kutumika kwa
kipindi cha miaka minane lakini baadaye kipindi hiki
kiliendelezwa hadi mwaka wa 2025. Fungu maalum pia kuhusiana na
nguo na mavazi yaliyotengenezwa viwandani liliongezwa kwa Sheria
ya AGOA, ambalo lilihitaji nchi ya Marekani inunue nguo
zilizotengenezwa viwandani kutoka katika nchi zinazostahiki
kufaidika na AGOA kabla ya kununua kutoka nchi nyingine. Sharti
hili la kupendelea nguo za nchi hizi zilizotengenezwa viwandani
limechangia bidhaa nje za Kenya nchini Marekani ziongezeke.
Kilichogunduliwa 5: Wanafunzi, wasomi na wafanyakazi – stadi wa Kenya hunufaika
kutokana na msaada wa kielimu na sera nzuri za uhamiaji za
Marekani ili kuendeleza kazi zao.
Ni muhimu kuwekeza katika wafanyakazi wa Kenya ili wapate ujuzi
mpya ambao ni muhimu katika jitahada za Kenya za kuwa na uchumi wa
kisasa ambao unaendeshwa na sekta ndogo ya kilimo lakini yenye
uzalishaji wa kiwango cha juu zaidi pamoja na ongezeko katika
uzalishaji wa viwanda. Ili kusaidia utimizaji wa lengo hili,
Serikali ya Marekani hufadhili fursa mbalimbali ili wanafunzi na
wasomi wa Kenya waweze kuendeleza mafunzo na elimu yao katika
taasisi za Marekani za elimu ya juu kupitia mipango yake ya viza
iliyoundwa kwa ajili ya wanafunzi (viza za F-1) na wasomi (viza za
J-1).
Mchoro wa 7
unaonyesha idadi ya jumla ya wanafunzi na wasomi wapya wa Kenya
wanaokwenda nchini Marekani kila mwaka kuanzia mwaka wa 2010 hadi
2018.
Mchoro wa 7. Idadi ya wanafunzi na wasomi wapya wa Kenya wanaokwenda
nchini Marekani, 2010-2018
↩
Maelezo: Grafu hii inaonyesha idadi ya wanafunzi na wasomi wapya
wa Kenya waliopatiwa viza za kuenda Marekani kati ya mwaka wa
2010 na 2018.
Asili: U.S. Department of State.
Mbali na kuwapatia Wakenya fursa za kupata stadi mwafaka
zinazohitajika ili kupata kazi zinazolipa vizuri, taasisi za
Marekani pia hukuza viongozi, watalaam na watu wabunifu wa kizazi
kijacho cha Kenya. Huku akiwa alihitimu kutoka Chuo cha Amherst
katika jimbo la Massachusetts katika mwaka wa 1985 akiwa na
shahada ya uchumi na elimu ya siasa, Rais Uhuru Kenyatta pengine
ndio Mkenya anayetambulika zaidi leo hii ambaye alipokea elimu ya
juu nchini Marekani.
Wanafunzi na wasomi wengi wa Kenya hupokea msaada wa kifedha
katika kipindi cha kusoma kwao kupitia misaada ya kulipiwa masomo
inayotolewa na mipango ya vyuo vikuu vya Marekani au mipango ya
serikali ya Marekani, kama vile Mpango wa Fulbright Scholarship au
Mpango wa Kimataifa wa Uongozi wa Wageni (the International
Visitors Leadership Program) (IVLP). Tunakadiria kwamba wanafunzi
na wasomi wa Kenya nchini Marekani hupokea angalau Dola milioni
19.6 kama msaada kila mwaka. Kiwango hiki tulichokadiria
kinatokana na kiwango wastani cha wanafunzi 400 wa Kenya ambao
walikuwa wakisomea shahada ya uzamivu katika Taasisi za Marekani
katika mwaka wowote kati ya mwaka wa 2014 na 2019.[18]
Wanafunzi wakenya ambao wanasomea shahada za uzamivu nchini
Marekani kwa kawaida hufadhiliwa kikamilifu na taasisi ambapo
wanasomea, ikiwemo karo, bima ya afya na hela za kujikimu za kila
mwezi.[19]
Hii ni sehemu ndogo tu ya jumla ya msaada wa kielimu unaotolewa na
Marekani kwa wanafunzi na wasomi wa Kenya, kwa vile wakenya
wengine ambao wanasomea viwango vingine vya elimu (k.m, shahada ya
kwanza, shahada ya uzamili, vyeti) pia wanaweza kupokea msaada wa
kifedha kutoka kwa taasisi za elimu ambapo wanasomea.
Ingawa wanafunzi na wasomi wengi hurudi nchini Kenya baada ya
kumaliza mipango yao ya elimu, baadhi yao huamua kujiunga na
wafanyakazi wa Marekani ili kufanya kazi za kitaalam kupitia
mpango wa viza ya H-1B. Mpango huu huwawezesha wafanyakazi wenye
ustadi wa hali ya juu wanaotoka kwenye nchi za kigeni kujiunga na
wafanyakazi wa Marekani na kupata ujuzi na uzoefu mwingine muhimu.
Kuanzia mwaka wa 2014 hadi wa 2018, serikali ya Marekani
ilipatiana viza 130 za H-1B kwa Wakenya kila mwaka. Huku kipindi
cha viza kikiwa cha miaka 6 kwa wastani na mshahara wa kila mwaka
ukiwa takriban Dola 80,600 kwa wapokeaji wa viza za H-1B,
tunakadiria kihafidhina kwamba raia wa kenya walipata karibu Dola
milioni 62.86 walipokuwa wameajiriwa nchini Marekeni.[20]
Kati ya mwaka wa 2009 na 2018, nchi ya Marekani ilipeana Ukaazi
Halali wa Kudumu (LPR), almaarufu Green Card, kwa Wakenya 70,136.
Watu ambao wana green card hii au hali hii halali wanastahiki
kupata fursa mbalimbali za kazi ambazo hutamaniwa na watu wengi
lakini haziwezi kupatikana na wahamiaji wengine. Kwa mujibu wa
takwimu za Idara ya Kudumisha Usalama Ndani ya Nchi ya Marekani,
Kenya iko kati ya nambari moja hadi tano miongoni mwa nchi za
Afrika zenye idadi kubwa ya walio na Green Card. Wakenya wengi
ambao ni LPRs na ambao ni wafanyakazi wa H-1B hudumisha uhusiano
thabiti na Kenya na huendelea kusaidia familia, marafiki na jamii
zao kwa kuwekeza kwenye biashara za Kenya na kwenye mali
zisizohamishika, pamoja na kutuma pesa nchini Kenya.
Kilichogunduliwa 6: Dhamana za bima ambazo zimeungwa mkono na Serikali ya Marekani
zimesaidia Kenya kuvutia takriban Dola milioni 742 ambazo
zimewekezwa kwenye sekta ya kibinafsi tangu mwaka wa 2010.
Ruwaza ya 2030 ya Kenya inatambua umuhimu wa kuvutia Uwekezaji wa
Kigeni wa Moja kwa Moja (FDI) ili kufadhili miundombinu ambayo
nchi inahitaji kabisa. Dhamana za bima ambazo zimeungwa mkono na
serikali ya Marekani huchangia pakubwa katika kuongeza imani ya
wawekezaji wa kigeni watarajiwa kupitia kupunguza vikwazo vya
kisiasa na kiuchumi vya kuwekeza katika uchumi wa Kenya.
Shirika la Marekani la Fedha na Maendeleo ya Kimataifa (The U.S.
International Development Finance Corporation) (DFC), lililokuwa
likijulikana hapo awali kama Shirika la Uwekezaji wa Kibinafsi Nje
ya Nchi (Overseas Private Investment Corporation, OPIC), ni wakala
huru ya serikali ambayo husaidia mashirika ya Kimarekani ambayo
yanataka kufanya biashara na kuwekeza katika nchi zinazoendelea.[21]
Kati ya mwaka wa 2010 na 2018, Serikali ya Marekani kupitia OPIC
ilitoa msaada wa kifedha kati ya nchi mbili na bima ya hatari kwa
ajili ya miradi 16 nchini Kenya, jumla ya fedha hizo ikiwa ni Dola
milioni USD 664 (takriban Dola milioni 74 kila mwaka). Kiwango
kikubwa cha fedha hizi kilichangia katika uwekezaji katika miradi
ya miundombinu ili kuongeza viwango vya nishati inayoweza kutumiwa
upya ambavyo Kenya inatoa (tazama
Mchoro wa 8), ikiwa ni pamoja na Mradi wa Nishati ya Upepo wa Kipeto na
upanuzi wa Stesheni ya Umeme wa Mvuke ya OrPower 4 (tazama Kikasha
cha 6). Miradi mingine ilichangia katika maendeleo ya kiuchumi kwa
kuimarisha ufikiaji wa huduma za benki, ujenzi wa shule na ujenzi
wa nyumba, na vipengele muhimu vya kilimo.
Mchoro wa 8. Dhamana za uwekezaji za Marekani kwenye sekta ya nishati na
sekta nyingine za Kenya, 2010-2018
↩
Asili: DFC (formerly OPIC) and MIGA, the World Bank.
Vile vile, Marekani pia imeunga mkono shughuli za Wakala wa
Kimataifa wa Udhamini wa Uwekezaji wa Benki ya Dunia (World Bank’s
Multilateral Investment Guarantee Agency, MIGA) za kupatiana
dhamana kwa mashirika yanayotaka kuwekeza nchini Kenya kutoka nchi
zenye uchumi ulionawiri na zenye uchumi unaokua kwa kasi. Kupitia
ufadhili wake muhimu kwa Jumuiya ya Maendeleo ya Kimataifa ya
Benki ya Dunia, Marekani imefadhili takriban asilimia 12 ya
dhamana za MIGA tangu 2010, ambayo ni Dola milioni 77 kati ya
jumla ya Dola milioni 840.3 zilizotolewa kwa ajili ya miradi ya
uwekezaji katika kipindi hicho (takriban Dola milioni 8.6 kwa
mwaka). Fedha hizo zilifadhili miradi ya nishati inayoweza
kutumika upya na isiyoweza kutumika upya pia, lakini nyingine
zilifadhili huduma za benki, fedha na biashara za kilimo.
Kupitia dhamana zake za OPIC na MIGA, serikali ya Marekani
imesaidia Kenya kuweza kuvutia Dola milioni 742 ambazo zimewekezwa
kwenye sekta ya kibinafsi tangu 2010.
Kikasha cha 6. Mradi wa Nishati ya Upepo wa Kipeto na Stesheni ya Umeme wa
Mvuke ya OrPower 4
↩
Mradi wa Nishati ya Upepo wa Kipeto na upanuzi wa Stesheni ya
Umeme wa Mvuke ya Olkaria III ndio miradi miwili kati ya mingine
yenye thamani ya juu kabisa inayofadhiliwa na dhamana za
uwekezaji za Marekani nchini Kenya, na yote miwili inadhihirisha
kwamba watendaji/watoa msaada wa Marekani na njia nyingine za
ufadhili za Marekani zimehusika. Kwa pamoja, miradi hii miwili
inachangia pakubwa katika kufanikisha malengo ya Ruwaza ya 2030
ya Kenya ya kuimarisha ufikiaji wa umeme na utengenezaji wa
vyanzo vipya vya nishati inayoweza kutumiwa upya (Ruwaza ya
2030).
Mradi wa Nishati ya Upepo wa Kipeto , ulioko kilomita 70 kusini
magharibi mwa Nairobi, umekuwa ndio pahali ambapo uwanja mkubwa
wa upepo umestahili kujengwa tangu serikali ya Ubelgiji
iliposakinisha tabo za upepo hapo katika mwaka wa 1993 (Power
Africa, 2019). Uwanja huo umeendelezwa sana hivi majuzi tu,
kutokana na ushirikiano kati ya General Electric na (GE) Kipeto
Energy Limited. Ushirikiano huu kati ya kampuni za Marekani na
Kenya uliweza kuvutia ufadhili wa OPIC wa Dola milioni 232.56
katika mwaka wa 2015 (ambazo zilifika Dola milioni 251.16 katika
mwaka wa 2019), takriban asilimia 72 ya gharama zote za mradi
huo (DFC, 2020). Huku ikiwa pia na Dola milioni 50 ya ziada ya
bima ya hatari iliyowekwa na OPIC katika mwaka wa 2018 (ambazo
zilifika Dola milioni 51 katika mwaka wa 2019), uwanja huu wa
upepo uliweka tabo ya kwanza ya upepo kati ya tabo 60 za GE
zinazopaswa kuwekwa mnamo Desemba 2019 (Kipeto Energy, 2019).
Ingawa ujenzi bado unaendelea, utakapokamilika, Uwanja wa Upepo
wa Kipeto utazalisha megawati 100 za umeme, zitakazotosha kutoa
umeme kwa nyumba 40,000 kwenye eneo hilo (General Electric,
2018).
Upanuzi wa stesheni ya umeme wa mvuke ya Olkaria III, iliyoko
kilomita 90 kaskazini magharibi mwa Nairobi, pia unaonyesha njia
nyingi ambazo Marekani inasaidia sekta ya nishati ya Kenya.
Katika mwaka wa 2011, OPIC ilipeana dhamana ya uwekezaji ya Dola
milioni 215.1 kwa Ormat Technologies (ambazo zilifika Dola
milioni 245.3 katika mwaka wa 2019) ili kufadhili upanuzi,
zikiambatana na dhamana ya uwekezaji ya MIGA ya Benki ya Dunia
ya Dola milioni 134 (ambazo zilifika Dola milioni 152.8 katika
mwaka wa 2019). Kutokana na msaada kutoka kwa dhamana hizi mbili
za ziada za uwekezaji, stesheni ya umeme ya Olkaria III
iliongeza kiwango cha nishati ambayo ilizalisha kutoka megawati
48 hadi megawati 84, kiwango ambacho karibu kiwe mara mbili ya
kiwango chake cha kawaida cha uzalishaji (World Bank, 2020).
Kwenye sura hii, tumeangazia njia tatu ambazo serikali ya Marekani
imetumia kuchangia maendeleo na ustawi wa Kenya. Hata hivyo,
ushirikiano kati ya Marekani na Kenya umehusisha usaidizi kutoka
kwa wengine ambao si serikali. Kwa kweli, Wahisani wa kibinafsi,
kampuni, mashirika yasiyo ya kiserikali ya Marekani na watu
binafsi wamekuza uhusiano wa karibu na washirika wao wa Kenya
katika miongo miwili iliyopita. Kwenye sura inayofuata,
tutazungumzia jinsi ambavyo mahusiano haya yanafaidi uchumi wa
Kenya na watu wake.