Sura ya Tano: Hitimisho
Katika ripoti hii, tuliuliza swali rahisi: Wakenya wanafahamu nini na wanachukulia aje ushirikiano wa nchi yao na Marekani?
Katika Sura ya 2, tulirekodi kwamba msaada unaoongozwa na serikali ya Marekani hutoa manufaa muhimu sana kwa watu wa Kenya, usaidizi wenyewe ukiwa wenye thamani ya Dola bilioni 1.68 kila mwaka. Marekani hupatiana usaidizi wake mwingi kupitia misaada rasmi wa maendeleo kati ya nchi mbili—ikiwemo ruzuku, mikopo yenye masharti bora, na ushauri wa kiufundi. Isitoshe, serikali ya Marekani imekuwa ikiunga mkono kwa dhati mashirika ya kimataifa (k.m., mashirika ya Umoja wa Kimataifa, benki za maendeleo) na hazina za wafadhili wengi zinazoendesha shughuli zao nchini Kenya. Hatimaye, pia tulijaribu kupima jinsi ambavyo sera nzuri za biashara, uhamiaji na uwekezaji za Marekani zinasaidia Kenya kujiboresha ili iiwe nchi inayoendelea kwa kasi yenye uchumi wa kipato cha kati ifikapo 2030.
Katika Sura ya 3, tuliangazia Dola bilioni 1.36 za ziada za kila mwaka zilizozalishwa kwa kukuza ushirikiano kati ya watendaji walioko kwenye kampuni, mashirika na watu binafsi ambao wanaendeleza maendeleo na ustawi wa Kenya. Kampuni za Marekani zinatoa nafasi za kazi, zinawekeza mtaji pamoja na kununua bidhaa na huduma ambazo zinaimarisha uchumi wa Kenya. Mashirika ya kihisani ya Marekani huchangia pesa kwenye sekta ya kibinafsi ili kuhimili gharama za serikali za kuwekeza katika raia na taasisi za Kenya, huku mashirika yasiyo ya kiserikali ya Marekani yakifanikisha miradi ambayo inaimarisha maisha moja kwa moja. Isitoshe, ulimwengu wetu unaozidi kuwa kama kijiji kimoja cha mataifa umewezesha michango kutoka wa watu binafsi kutoka Marekani na utoaji wa mikopo midogo midogo kupitia mitandao ya kuchangisha fedha, mapato kutoka kwa watalii wa Marekani wanaozuru nchi ya Kenya na pesa zinazotumwa na Wakenya wanaofanya kazi nchini Marekani.
Yote kwa pamoja, tunakadiria kwamba ushirikiano kati ya Marekani na Kenya huchangisha takriban jumla ya Dola bilioni 3.05 kila mwaka ili kufadhili maendeleo na ustawi wa Kenya. Katika Sura ya 4, tuliangazia jinsi ambavyo usaidizi wa Marekani unaweza kusaidia Kenya kutimiza malengo yake mahususi ya kiuchumi, kijamii na kiutawala sambamba na ajenda yake ya Ruwaza ya 2030. Pia tulijifunza kwamba viongozi wengi wa Kenya walioulizwa maswali walisema kwamba Marekani inahusika kiutendaji na inatoa mchango mkubwa katika maendeleo ya nchi yao, ijapokuwa, wananchi wanaamini zaidi kwamba mfumo wa maendeleo wa Marekani ndio ulio bora zaidi wa kuigwa, kuliko jinsi ambavyo viongozi wanaamini.
Kwa vile ni vigumu sana kutaja viwango kamili vya uwekezaji na michango ya kifedha isiyo rasmi, takwimu zilizoko kwenye ripoti hii ni vya kukadiriwa tu, na jumla ya mchango wa Marekani katika maendeleo na ustawi wa Kenya huenda, kwa kweli, ikawa kubwa zaidi. Hata hivyo, tunatumai kwamba ripoti hii imetoa msingi muhimu wa kuwasaidia wananchi na viongozi wa Kenya kutathmini wenyewe thamani ya ushirikiano wa nchi yao na Marekani.