Muhtasari

Marekani ni mshirika muhimu katika azma ya Kenya ya kutimiza Ruwaza yake ya 2030, lakini ni taarifa chache ambazo Wakenya wanaweza kupata ili kuwawezesha kutathmini thamani ya ushirikiano huu katika maisha yao ya kila siku. Ripoti hii inachunguza faida za ushirikiano kati ya Kenya na Marekani katika ukuaji na ustawi wa Kenya kwa msingi wa mtazamo wa jamii nzima. Kwa pamoja, mawakala wa serikali ya Marekani, mashirika na watu binafsi huchangia takriban Dola bilioni 3.05 kila mwaka (KSH B 310) katika maendeleo ya Kenya.

Serikali ya Marekani huchangia takriban Dola bilioni 1.68 kila mwaka (KSH B 171), ikitilia mkazo sana sekta za afya, usalama, utawala na miundombinu. Mchango huo unajumuisha msaada wa moja kwa moja kati ya nchi mbili (Dola milioni 931) na misaada ya kimataifa (Dola milioni 73.5), na pia Dola milioni 678 katika michango isiyo ya moja kwa moja kutoka kwa biashara saidizi, uhamiaji, na sera za uwekezaji.

Vyanzo visivyo vya kiserikali vya Marekani huchangia takriban Dola bilioni 1.36 kila mwaka (KSH B 139). Hiyo ni pamoja na: Dola milioni 517.6 kupitia fedha zinazotumwa na Wakenya wanaofanya kazi nchini Marekani, Dola milioni 294.2 katika uwekezaji wa kigeni wa moja kwa moja, Dola milioni 270 katika shughuli za mashirika yasiyo ya kiserikali, Dola milioni 190.7 kupitia mtiririko wa fedha kutokana na shughuli za kitalii, Dola milioni 87.3 kutoka kwa mifuko ya kibinafsi, na Dola milioni 4.6 katika mikopo midogo na michango ya kibinafsi.

Mbali na faida hizi za kifedha, ushirikiano wa Kenya na Marekani huchangia katika ukuaji na ustawi kupitia njia nyingine zinazoweza kuonekana:

  • Msaada wa Marekani unaolenga afya hausaidii tu kuokoa maisha ya watu, bali pia unachangia katika uzalishaji wa kiuchumi wa Kenya kadiri watu wanavyoendelea kufanya kazi kwa muda mrefu zaidi. Kama mtoaji mkubwa zaidi wa fedha zinazohusiana na HIV/UKIMWI (Dola bilioni 4.5 kati ya 2009-2018), Marekani imehamasisha rasilimali na utaalamu wa kusaidia wafanyakazi wa afya wa mstari wa mbele katika juhudi zao za kupambana na janga la UKIMWI. Tunakadiria kuwa juhudi hizi zimesaidia kuokoa maisha ya watu zaidi ya milioni moja hadi kufikia leo. Kadiri umri wa kuishi unavyoongezeka, ndivyo miaka ya uzalishaji wa kiuchumi ya Mkenya wa kawaida inaongezeka kwa miaka 15.
  • Katika kuelekeza takriban Dola milioni 19.6 kila mwaka (KSH B 2) katika msaada unaolenga utawala, Marekani inasaidia maafisa wa Kenya kuboresha jinsi wanavyotoa huduma na kushughulikia mahitaji ya raia. Utafiti wa hivi karibuni wa Afrobarometer unaonyesha kwamba kadiri Kenya inavyozidi kutoa nafasi kwa idadi inayoongezeka ya vyama mbalimbali vya kisiasa na raia wanavyoendelea kuhakikisha sauti zao zinasikika kupitia kupiga kura, ndivyo familia zitakavyozidi kuwa na matumaini zaidi na uwezo wa serikali yao katika kutoa huduma muhimu kwa uaminifu na kwa usawa. Kwa mfano, kumekuwa na ongezeko la asilimia 15 katika idadi ya nyumba zinazoweza kufikia maji safi na ongezeko la asilimia 40 katika idadi ya nyumba zinazoweza kufikia umeme kati ya miaka ya 2000 na 2017.
  • Msaada wa Marekani unaolenga kilimo unasaidia kuongeza uzalishaji katika maeneo ya mashambani ya Kenya kupitia kupunguza hatari zinazohusiana na hali ya hewa, kuongeza mapato ya uuzaji, na kuboresha ufikiaji wa soko. Kilimo kilizalisha asilimia 34 ya Pato la Taifa (GDP) linalozidi kuongezeka mnamo 2018, kutoka asilimia 22 mnamo 2008. Wakati huo huo, mapato ya wastani ya kila raia yameongezeka kwa njia thabiti tangu 2008 na ukosefu wa usawa katika mapato umepungua tangu miaka ya 1990. Kwa kuwa 3/4 ya idadi ya watu wa Kenya hutegemea kilimo kwa kiasi fulani au kikamilifu kwa ajili ya kujikimu kimaisha, kuna uwezekano kwamba baadhi ya manufaa hayo yametokea kwa ajili ya ongezeko katika uzalishaji wa kilimo na mapato husiani.