← Kuhusu ripoti

Kuwekeza kwa Watu wa Tanzania:

Kuthamini Ushirikiano wa Marekani na Tanzania kwa Maendeleo

Mei 2024

Divya Mathew, Bryan Burgess, Samantha Custer, Rodney Knight, Kelsey Marshall, Lucas Katera, Jane Mpapalika, Constantine George Simba na Cornel Jahari

Muhtasari Mahsusi

Nchi ya Marekani ni mshirika mkuu wa Tanzania. Uhusiano kati ya nchi hizi mbili umejengwa katika mihimili mitatu: diplomasia, maendeleo na ulinzi. Hata hivyo, kuna taarifa chache zinazopatikana kwa Watanzania kwa urahisi ili kuwawezesha kutathmini thamani ya ushirikiano huo katika maisha yao ya kila siku, hasa wanapopima maendeleo ya kufikia malengo ambayo nchi imejiwekea katika Dira ya Maendeleo ya Tanzania ya mwaka 2025. Ripoti hii inabainisha jinsi ambavyo ushirikiano wa Marekani na Tanzania unachangia ukuaji na mafanikio ya Tanzania—kupitia rasilimali zinazokusanywa na matokeo yanayotokana na rasilimali hizo.

Watafiti wamezingatia maoni ya jamii nzima kwa kuchunguza sio tu msaada rasmi wa maendeleo bali pia michango ya sekta binafsi kupitia biashara, utalii, uwekezaji, hisani, na miamala mbalimbali. Utafiti huu unachanganua historia ya mtiririko wa fedha kutoka vyanzo vya Marekani kwenda Tanzania kwa takriban muongo mmoja, kuanzia 2012 hadi 2022. Pia, utafiti unahusisha maoni ya viongozi wa umma, sekta binafsi na mashirika ya kiraia jinsi wanavyotathmini ushirikiano huo kwa sasa kupitia dodoso na usaili. Uchambuzi wa data ulifanywa na AidData- Maabara ya Taasisi ya Kimataifa ya Utafti ya William & Mary ya nchini Marekani kwa ushirikiano na REPOA- Shirika la Utafiti wa Sera Tanzania.

Kuhusiana na fedha, mashirika ya serikali ya Marekani, kampuni na watu binafsi kwa pamoja huchangia takribani dola bilioni 2.8 kila mwaka (TZS Bn 7,140) kwa ajili ya maendeleo ya Tanzania. Serikali ya Marekani inachangia takribani dola bilioni 1.0 kila mwaka (TZS Bn 2,550), katika sekta ya afya, kilimo na miundombinu. Mnamo 2022, hii ni pamoja na misaada ya moja kwa moja ya makubaliano ya nchi na nchi na misaada ya kimataifa (USD milioni 824.2) na mchango wa sera za biashara na uwekezaji (USD milioni 205.3). Vyanzo vya Marekani ambavyo si vya wakala wa serikali vinachangia takribani dola bilioni 1.8 kila mwaka (TZS Bn 4,590) kupitia uwekezaji wa kigeni wa moja kwa moja (USD bilioni 1.3), fedha kutoka kwa Watanzania wanaofanya kazi Marekani (USD milioni 103.7), mapato ya utalii (USD milioni 317.7), na mashirika binafsi (USD milioni 96.3), pamoja na michango ya mtu mmojammoja na mikopo midogomidogo (USD milioni 0.3). Pamoja na manufaa hayo ya kifedha, ushirikiano wa Marekani na Tanzania unachangia ukuaji na ustawi wa jamii kwa njia mbalimbali: