Kilichogunduliwa 2: Marekani ilielekeza Dola milioni 95.6 kwa wastani katika msaada wake wa kila mwaka kati ya mwaka wa 2014 na 2018 kusaidia Kenya kukabiliana na ugaidi, kuhakikisha usalama wa mpaka wake, na kutekeleza sheria za nchi kwa njia mwafaka.

Kati ya 2010 na 2018, mawakala wanane wa serikali ya Marekani kwa pamoja walitoa wastani wa Dola milioni 705.1 katika msaada wa kiuchumi na kijeshi (asilimia 31 na asilimia 69, mtawalia) ili kusaidia mageuzi katika sekta ya usalama ya Kenya, kukuza amani, na juhudi za usimamizi wa migogoro.[7] Sehemu kubwa ya msaada huu (asilimia 53) ililenga kuimarisha uwezo wa nchi ya Kenya kukabiliana na vitisho vya kigaidi kutoka Al Shabaab, kikundi cha waasi cha Somali kinachoshirikiana na Al Qaeda, na kuboresha usalama wa mpaka (tazama Mchoro wa 4). Katika miaka mitano iliyopita, Marekani imeelekeza wastani wa Dola milioni 95.6 kwa mwaka wa msaada wake kati ya nchi mbili katika amani na usalama wa Kenya kwa jumla.[8]

Mpango wa Global Train and Equip, ambayo "hutoa mafunzo, huduma, na vifaa kwa huduma za usalama za kitaifa," imekuwa msingi muhimu wa ushirikiano katika ya Marekani na Kenya katika masuala ya usalama tangu 2011 (DSCA, 2020). Ikichangia Dola milioni 329.9 (asilimia 47) katika msaada wote wa Marekani unaolenga amani na usalama kati ya mwaka wa 2010 na 2018, mpango huo umewezesha huduma za usalama za Kenya kupata vifaa (kwa mfano, helikopta, ndege zisizokuwa na rubani), mafunzo ya operesheni maalum za usalama, na msaada wa kiufundi ili kuwezesha Kenya kuchangia kwa njia fanisi katika Misheni ya Umoja wa Afrika nchini Somalia ikishirikiana na nchi nyingine nne zilizopeleka wanajeshi wake nchini humo.

Kutilia mkazo uimarishaji wa utendakazi wa idara ya polisi ya Kenya na jeshi la Kenya si jambo linalozingatiwa na mpango wa Global Train and Equip pekee. Serikali ya Marekani ilitoa mafunzo kwa maafisa 3,407 wa sekta ya usalama ya Kenya kati ya mwaka wa 2010 na 2018 katika mipango 15 tofauti, ikizingatia mada kama vile kupambana na ugaidi na shughuli za kulinda amani pamoja na utekelezaji wa sheria za baharini na vita dhidi ya dawa za kulevya. Kwa mujibu wa ripoti moja ya mwaka wa 2019, thamani ya Dola ya mipango ya mafunzo iliyotolewa kwa wafanyakazi wa sekta ya usalama ya Kenya katika mwaka wa fedha wa 2018 pekee ilikuwa takriban Dola milioni 4.9.[9] Jedwali la 2 linaonyesha idadi inayokadiriwa ya Wakenya waliopokea mafunzo kupitia mipango ya msaada wa usalama iliyowezeshwa na serikali ya Marekani kati ya mwaka wa 2010 na 2018.

Mchoro wa 4. Michango ya Marekani katika usalama wa Kenya, kukuza amani, na usimamizi wa migogoro, 2010-2018

Nyinginezo Vita dhidi ya silaha za maangamizi (Weapons of Mass Destruction, WMD) Kupunguza athari za migogoro na maridhiano Shughuli za Udhibiti na mageuzi katika sekta ya usalama Vita dhidi ya ugaidi $ milioni 374.7 143.7 80.6 78.4 27.8

Asili: Foreign Aid Explorer (2010-2018).

Jedwali la 2. Wafanyakazi wa sekta ya usalama ya Kenya waliofunzwa kwa mtazamo wa mpango, 2010-2018

Jina la mpango wa mafunzo Wakenya waliofunzwa, 2010-2018
Shughuli za Kulinda Amani 806
Mafunzo Yanayosimamiwa na Mamlaka Moja 676
Vituo vya Kanda vya Mafunzo ya Usalama 451
Uuzaji wa Vifaa vya Kijeshi Katika Nchi za Nje -- Mafunzo Yanayohusiana na Ununuzi wa vifaa 304
Sehemu ya 1206 ya Mamlaka ya Mafunzo na Zana 284
Elimu na Mafunzo ya Kijeshi ya Kimataifa 268
Mpango wa Mafunzo ya Kupambana na Ugaidi 230
Sehemu ya 333 ya Kuimarisha Uwezo wa Mshiriki 186
Shughuli za Marekani za Mafunzo ya Walinzi wa Pwani 126
Ufadhili wa Kifedha wa Jeshi la Kigeni -- Mafunzo na Elimu ya Kijeshi kati ya Nchi Mbili 40
Hazina ya Ushirikiano wa Kupambana na Ugaidi 17
Sehemu ya 1004 ya Kupambana na Dawa za Kulevya 10
Mafunzo ya Kuhudumu katika Jeshi (Jeshi la Marekani, Wanamaji, Wanahewa) 4
Mpango wa Uongozi wa Wanahewa 3
Mafunzo ya Kubadilishana 2

Asili: Security Assistance Monitor (2010-2018).

Kilichogunduliwa 3: Serikali ya Marekani ilichangia takriban Dola milioni 73.5 kwa mwaka kwa wastani kwa Kenya kupitia ushirikiano wa kimataifa, haswa katika sekta za afya, utawala, na miundombinu.

Katika miaka ya hivi karibuni, Marekani imetoa kiasi kinachoongezeka cha msaada wake rasmi wa jumla wa maendeleo kupitia mashirika ya kimataifa (kwa mfano, mashirika ya Umoja wa Mataifa, benki za maendeleo za kanda) na hazina za wafadhili wengi zinazohusiana na vipaumbele vya sekta maalum (Pipa et al., 2018). Hata hivyo, michango ya Marekani ya kibinafsi imefichika kwa sababu mashirika ya kimataifa huchanganya msaada wa kifedha wa Marekani na michango ya wafadhili wengine.

Mbali na mpango wake wa msaada kati ya nchi mbili, serikali ya Marekani ilichangia wastani wa takriban Dola milioni 73.5 kwa mwaka [10] kwa Kenya kati ya 2014 na 2018, kupitia msaada wake wa msingi kwa mashirika 20 ya kimataifa yanayofanya kazi nchini Kenya (tazama Mchoro wa 5). [11] Katika miaka mitano iliyopita, sehemu kubwa ya michango ya Marekani kupitia mashirika ya kimataifa na hazina zinazofanya kazi nchini Kenya ilikuwa katika sekta ya afya (asilimia 62) na sekta ya miundombinu (asilimia 12). Takwimu hizi hazijumuishi michango ya serikali ya Marekani kwa mashirika ya kiserikali ya kikanda kama vile Soko la Pamoja la Afrika Mashariki na Kusini (COMESA), Jumuiya ya Afrika Mashariki (East Africa Community) au Jumuiya ya Mamlaka ya Kimataifa kuhusu Maendeleo (Inter-governmental Authority on Development, IGAD), ambayo yanajadiliwa kando katika Kikasha cha 4.

Kukadiria michango ya Marekani kwa mashirika na hazina za kimataifa kwa msingi wa sekta mahususi kunategemea sekta inayotiliwa mkazo na kila taasisi. Michango ya serikali ya Marekani ya kila mwaka kupitia Benki ya Dunia (Dola milioni 15.74) [12] na Benki ya Maendeleo ya Afrika (Dola milioni 1.42), [13] kwa mfano, hunufaisha kwa kiwango kikubwa miundombinu na tasnia za Kenya, nishati, na sekta za usambazaji wa maji na usafi wa mazingira, kulingana na majukumu ya mashirika hayo mawili. Jumuiya ya Kimataifa ya Maendeleo ya Benki ya Dunia (IDA)—ambayo hutoa mikopo na msaada ili kukuza maendeleo ya kiuchumi, kupunguza ukosefu wa usawa, na kuboresha hali ya maisha ya watu—imezidi kufadhili miradi ya utawala bora, kama vile kuboresha utawala wa umma wa Kenya kupitia mradi wake wa National Safety Net Program for Results.

Marekani ilifadhili takriban asilimia 18 (Dola milioni 6.44) ya shughuli za Umoja wa Mataifa nchini Kenya kila mwaka kati ya mwaka wa 2014 na 2018. [14] Msaada huu wa msingi unafadhili mashirika 12 ya Umoja wa Mataifa yanayofanya kazi nchini Kenya kwa kutilia mkazo sekta mbili: (1) kilimo na uhakika wa chakula (Dola milioni 3.2 kwa mwaka) na (2) mizozo, vita, na mwitikio wa mahitaji ya kibinadamu (Dola milioni 1.4 kwa mwaka). Juhudi hizi zinaenda sambamba na msaada kati ya nchi mbili ambayo Marekani huelekeza katika maendeleo ya kilimo na kukabiliana na ukame. Kwa mfano, msaada wa Marekani kwa mashirika ya kimataifa kama vile Shirika la Chakula na Kilimo (Food and Agricultural Organization, FAO) husaidia miradi ambayo inasaidia Kenya na nchi nyingine katika kanda ya Afrika Mashariki kupambana kwa njia endelevu na nondo, nzige, na wanyama wengine waharibifu ambao ni tishio kwa mazao ya kilimo.

Shirika la Chakula Duniani (WFP) ndilo mpokeaji mkubwa zaidi wa msaada wa Marekani kati ya mashirika yote ya Umoja wa Mataifa, ambao ni asilimia 38 ya jumla ya ufadhili ambao shirika hilo hutoa kwa nchi ya Kenya. Msaada wa wastani wa kila mwaka wa Marekani wa Dola milioni 4.1 kwa WFP ni karibu mara 2.7 ya fedha zinazotolewa na mfadhili wa pili kwa ukubwa, na msaada huo huchangia katika kukuza kipaumbele cha maendeleo cha Kenya cha uhakika wa chakula.

Kwa kuongezea, Marekani huchangia takriban Dola milioni 49.85 kwa mwaka kwa hazina nyingine tano za kimataifa zinazofanya kazi nchini Kenya.[15] Hazina ya Dunia (Global Fund) na Ushirika wa Kimataifa wa Chanjo (GAVI) hupokea asilimia 96 ya michango hiyo (Dola milioni 43.02 kwa mwaka), sambamba na mkazo mkubwa ambao msaada wa Marekani kati ya nchi mbili umeweka katika kupambana na magonjwa ya kuambukiza (HIV/UKIMWI, malaria, na kifua kikuu). Kupitia Hazina ya Kukabiliana na Hali za Dharura (Central Emergency Response Fund, CERF), Hazina za Uwekezaji katika Masuala ya Hali ya Hewa (Climate Investment Funds, CIFs) na Hazina ya Mazingira ya Kimataifa (GEF), Marekani ilichangia wastani wa Dola milioni 6.83 kila mwaka katika kukabiliana na majanga ya kimazingira, ulinzi wa mazingira, kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa, na miradi ya nishati inayoweza kutumika upya.

Hatimaye, Marekani pia ilichangia katika ruzuku ya Dola milioni 53.8 kama sehemu ya Dola milioni 909.6 zilizotolewa kwa Kenya kama mikopo yenye masharti mazuri na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) kati ya 2009 na 2013, kwa wastani wa Dola milioni 10.8 kwa mwaka wakati wa kipindi hicho.[16]

Mchoro wa 5. Makadirio ya kila mwaka ya mgawo wa Marekani katika matumizi ya kimataifa ya fedha kwa mtazamo wa mawakala, 2014-2018

Benki ya Maendeleo ya Afrika Mawakala wa Umoja wa Mataifa CERF, CIF, GEF Benki ya Dunia GAVI & Hazina ya Dunia $ milioni 43.0 15.7 6.8 6.4 1.4

Maelezo: Grafu hii inaonyesha mgawo unaokadiriwa wa kila mwaka wa matumizi ya kimataifa ya fedha ambao unaweza kuhusishwa na Marekani kwa msingi wa data ya miaka ya 2014-2018. Thamani za fedha zimewekwa kwa msingi wa thamani isiyobadilika ya Dola ya 2019.

Asili: OECD CRS Database, calculations by AidData.

Kikasha cha 4. U.S. assistance to regional intergovernmental organizations

Pamoja na taasisi na hazina za kimataifa zilizoelezwa katika sehemu ya 2.1, Marekani hutoa msaada kwa mashirika kadhaa ya kiserikali ya kikanda na Kenya ni nchi wanachama wa mashirika hayo. Kati ya mashirika hayo, matatu makubwa zaidi, kwa msingi wa msaada uliotolewa na Marekani kati ya kati ya 2001 na 2018, ni: Soko la Pamoja la Afrika Mashariki na Kusini (COMESA), Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), na Jumuiya ya Mamlaka ya Kimataifa kuhusu Maendeleo (IGAD).

Marekani ilitoa msaada wa Dola milioni 47.5 kusaidia kanda hiyo kupitia COMESA kati ya 2001 na 2018, na asilimia hamsini na tisa ya msaada huo ulilenga kilimo na uhakika wa chakula. Kati ya mwaka wa 2010 na 2018, serikali ya Marekani ilitoa msaada wa Dola milioni 25.3 kupitia Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC). Robo tatu ya dola hizo za msaada ziligawanywa katika nyanja zifuatazo: Kilimo na uhakika wa chakula (asilimia 24), ukuaji wa kiuchumi na biashara (asilimia 25), na mazingira (asilimia 27). Wakati huo huo, Marekani ilitenga zaidi ya nusu (asilimia 52) ya Dola milioni 21.3 ya msaada wake kwa IGAD kusaidia kanda hiyo kushughulikia mizozo na vita.

Hatukujumuisha michango kwa mashirika ya kiserikali ya kikanda katika takwimu za jumla za msaada wa kimataifa, kwa kuwa takwimu hizo hazikuwa maalum kwa Kenya; hata hivyo, kuna uwezekano kwamba michango hiyo bado inaweza kuleta mtiririko wa faida kwa Kenya.