Sura ya Kwanza Utangulizi

Kenya inaazimia kuwa "taifa lenye ushindani na ustawi wa viwango vya kimataifa na lenye kiwango cha juu cha ubora wa maisha ifikapo mwaka wa 2030" (Mpango wa Kwanza wa Muda wa Kati, 2008-2012). Ili kufanikisha maono hayo ya kiwango cha juu, Kenya lazima iendeleze miundombinu yake ili iwe ya kisasa, iongeze utengenezaji wa bidhaa na mauzo ya nje, na ifuate mifumo mwafaka ya utawala ili kuhakikisha kuwa raia wote wananufaika kutokana na maendeleo ya kiuchumi ya Kenya.[1]

Ushirikiano wa kimkakati na marafiki kama Marekani ni muhimu katika jitihada za Kenya za kufikia Ruwaza yake ya 2030. Kwa zaidi ya miaka 50[2], serikali ya Marekani imewekeza katika watu na taasisi za Kenya, ikishirikiana na umma, asasi za kiraia, na watendaji wa sekta ya kibinafsi. Licha ya hiyo, michango ya Marekani katika maendeleo ya Kenya ni zaidi ya msaada kutoka kwa serikali ya Marekani pekee. Kampuni za Marekani, vyuo vikuu, mashirika ya hisani, mashirika yasio ya kiserikali (NGOs), na watu binafsi wamezidi kushirikiana na wenzao nchini Kenya kwa miongo kadhaa iliyopita.

Licha ya uhusiano huu wa muda mrefu, viongozi wa Kenya na umma hawawezi kupata taarifa kwa urahisi ili kutathmini thamani ya ushirikiano wa nchi yao na Marekani.[3] Ingawa ni vigumu kuonyesha manufaa yote ambayo Kenya imepata kutokana na uhusiano wake na Marekani, ripoti hii inatoa makadirio ya kihafidhina ya michango ya Marekani katika ukuaji na ustawi wa Kenya, ikiwemo michango kutoka kwa watendaji wa kiserikali na wasio wa kiserikali. Kwa kiwango cha chini, tunakadiria michango hiyo kwa jumla kuwa takriban Dola bilioni 3.05 kila mwaka, kwa wastani (tazama Jedwali la 1).

Katika sura ya pili, tunatathmni takriban Dola bilioni 1 kwa mwaka kwa wastani katika michango ya moja kwa moja kutoka kwa serikali ya Marekani ili kusaidia mpango wa Ruwaza ya 2030 ya serikali ya Kenya. Pia tunatathmini wastani wa takriban Dola milioni 678 kwa mwaka ambayo serikali ya Marekani imehamasisha kwa njia isiyo ya moja kwa moja kupitia sera na taasisi za ndani zinazofaidi Kenya.

Katika sura ya tatu, tunahesabu takriban Dola bilioni 1.36 kwa wastani kwa mwaka katika michango kutoka kwa watu, mashirika, na kampuni za Marekani katika ustawi wa Kenya. Michango hii ni ya aina mbalimbali, kuanzia vitendo vya watu binafsi (k.m. utalii, fedha zinazotumwa nchini Kenya, michango ya kibinafsi) hadi juhudi za kitaasisi zaidi (k.m., misaada kutoka kwa mashirika ya ufadhili ya Marekani, shughuli za mashirika yasiyo ya kiserikali ya Marekani, uwekezaji wa kigeni wa moja kwa moja).

Katika sura ya nne, tunachambua matokeo ya utafiti wa AidData 2020 wa viongozi wa Kenya wa sekta ya umma na ya kibinafsi pamoja na viongozi wa asasi za kiraia ili kuelewa jinsi wanavyotathmini ushirika wa nchi yao na Marekani. Pia tutatathmini manufaa za kiuchumi, kijamii na za kiutawala zinazoweza kupatikana katika siku za usoni kutokana na shughuli za Marekani nchini Kenya. Tunatamatisha katika sura ya tano kwa kurudia kimuhtasari mambo makuu ya kutia akilini kutoka kwa utafiti huu.

Jedwali la 1. Muhtasari wa makadirio ya kila mwaka ya michango ya Marekani katika ukuaji na ustawi wa Kenya, mamilioni ya Dola/KSH

Michango Dola KSH
Msaada kati ya nchi mbili Dola 931.0 Ksh 94,721.3
Msaada wa kimataifa Dola 73.5 Ksh 7,473.3
Michango ya Marekani ya Moja kwa Moja Dola 1,004.5 Ksh 102,194.6
Biashara Dola 576.2 Ksh 58,622.6
Dhamana za uwekezaji Dola 82.4 Ksh 8,387.1
Msaada wa masomo Dola 19.6 Ksh 1,994.1
Faida za sera za Marekani Dola 678.2 Ksh 69,003.8
Michango ya serikali ya Marekani Dola 1,682.7 Ksh 171,198.4
Fedha zilizotumwa nchini Kenya Dola 517.6 Ksh 52,660.2
Uwekezaji wa kigeni wa moja kwa moja Dola 294.2 Ksh 29,931.7
Shughuli za mashirika yasiyo ya kiserikali ya Marekani Dola 270.0 Ksh 27,469.8
Utalii Dola 190.7 Ksh 19,406.7
Michango ya Hisani Dola 87.3 Ksh 8,882.0
Mikopo midogo Dola 4.2 Ksh 427.3
Michango ya kibinafsi Dola 0.4 Ksh 39.0
Michango ya jamii ya Marekani Dola 1,364.4 Ksh 138,816.7
Jumla ya Michango ya Marekani Dola 3,047.1 Ksh 310,015.1

Maelezo: Jedwali hili linaonyesha wastani wa michango kutoka Marekani katika ukuaji na ustawi wa Kenya kwa msingi wa thamani isiyobadilika ya Dola ya mwaka wa 2019 kwa kila kategoria. Tulipiga hesabu ya kadirio la mchango wa kila mwaka kwa kila aina ya msaada kwa kuchukua wastani wa miaka yote ya data inayopatikana kati ya mwaka wa 2014 na 2018, ila hatukuzingatia masuala yote. Idadi ya miaka iliyotumiwa kupiga hesabu ya wastani ilibadilika kulingana na idadi ya miaka iliyopatikana katika asili ya data. Kiwango cha ubadilishaji wa sarafu cha Dola 1 = 101.74 KSH kilitumiwa.

Asili: Makadirio ya AidData. Tazama Kiambatisho cha Kiufundi kinachoambatana na ripoti hii kwa maelezo zaidi.